Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 13

Matendo 13:18-42

Help us?
Click on verse(s) to share them!
18Aliwavumilia kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani.
19Aliyaangamiza mataifa ya nchi ya Kanaani akawapa hao watu wake ile nchi kuwa mali yao.
20Miaka mia nne na hamsini ilipita, halafu akawapatia waamuzi wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samweli.
21Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa Saulo, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka arobaini.
22Baada ya kumwondoa Saulo, Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme wao. Mungu alionyesha kibali chake kwake akisema: Nimemwona Daudi mtoto wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote ninayotaka kuyatenda.
23Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu.
24Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa.
25Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.
26“Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.
27Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi. Wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo.
28Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe.
29Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini.
30Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu.
31Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli.
32Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu.
33Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili: Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.
34Na juu ya kumfufua kutoka wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.
35Naam, na katika sehemu nyingine za zaburi asema: Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.
36Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza mapenzi ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza.
37Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza.
38Jueni wazi, ndugu zangu, kwamba ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu kwa njia ya Yesu Kristo;
39na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya Sheria ya Mose.
40Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii:
41Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni.”
42Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika ile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo.

Read Matendo 13Matendo 13
Compare Matendo 13:18-42Matendo 13:18-42