Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 10

Matendo 10:3-31

Help us?
Click on verse(s) to share them!
3Yapata saa tisa mchana, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!”
4Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini.
5Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.
6Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.”
7Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu,
8akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa.
9Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali.
10Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, alipatwa na usingizi mzito akaona maono.
11Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne.
12Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani.
13Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!”
14Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.”
15Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!”
16Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.
17Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hilo maono alilokuwa ameliona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni,
18Wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?”
19Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa lile maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! kuna watu watatu hapa, wanakutafuta.
20Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.”
21Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?”
22Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.”
23Petro akawaalika ndani, akawapa mahali pa kulala usiku ule. Kesho yake, Petro alianza safari pamoja nao, na baadhi ya ndugu wa huko Yopa walifuatana naye.
24Siku ya pili yake, walifika Kaisarea na huko Kornelio alikuwa anawangojea pamoja na jamaa na marafiki aliokuwa amewaalika.
25Petro alipokuwa anaingia, Kornelio alitoka nje kumlaki, akapiga magoti mbele yake na kuinama chini kabisa.
26Lakini Petro alimwinua, akamwambia, “Simama, kwa maana mimi ni binadamu tu.”
27Petro aliendelea kuongea na Kornelio wakiwa wanaingia nyumbani ambamo aliwakuta watu wengi wamekusanyika.
28Petro akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua kwamba Myahudi yeyote amekatazwa na Sheria yake ya dini kushirikiana na watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amenijulisha nisimfikirie mtu yeyote kuwa najisi au mchafu.
29Kwa sababu hiyo, mliponiita nimekuja bila kusita. Basi, nawaulizeni: kwa nini mmeniita?”
30Kornelio akasema, “Siku tatu zilizopita saa kama hii, saa tisa alasiri, nilikuwa nikisali chumbani mwangu. Ghafla, mtu aliyekuwa amevaa mavazi yenye kun'gaa alisimama mbele yangu,
31akasema: Kornelio! Sala yako na sadaka zako kwa maskini vimekubaliwa na Mungu.

Read Matendo 10Matendo 10
Compare Matendo 10:3-31Matendo 10:3-31