Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mambo ya Walawi - Mambo ya Walawi 19

Mambo ya Walawi 19:13-34

Help us?
Click on verse(s) to share them!
13Usimgandamize jirani yako wala kumwibia. Usishikilie malipo ya kibarua usiku kucha hata asubuhi.
14Usimlaani kiziwi au kuweka kikwazo mbele ya kipofu. Badala yake, yakupasa umwogope Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh.
15Usisababishe hukumu ikawa ya uongo. Usionyeshe upendeleo kwa mtu fulani eti kwa kuwa tu yeye ni masikini na usionyeshe upendeleo kwa mtu fulani eti kwa kuwa tu yeye ni mtu muhimu. Badala yake, amua juu ya jirani yako kwa haki.
16Usiende huku na huko ukisema habari za uchochezi miongoni mwa watu wako, bali tafuta kuyalinda maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Yahweh.
17Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Mkemee jirani yako kwa heshima ili kwamba usishiriki katika dhambi kwa sababu yake.
18Usijilipize kisasi au kuwa na chuki yoyote dhidi ya mtu yeyote wa watu wako, lakini badala yake mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Yahweh.
19Shika amri zangu. Usiwazalishe wanyama wako kwa kutumia wanyama wa aina nyingine tofauti. Usichanganye aina mbili tofauti za mbegu unapopanda shamba lako. Usivae vazi lililofumwa kwa kutumia nyuzi za rangi mbili tofauti zilizochanganywa pamoja.
20Yeyote anayelala na msichana mtumwa aliyeposwa na mume mwingine, lakini ambaye hajakombolewa au hajaachwa huru, lazima waadhibiwe. Hawatauawa kwa sababu yule msichana hakuwa huru.
21Ni lazima mtu huyo alete sadaka yake ya hatia kwenye ingilio la hema la kukutania—kondoo dume iwe sadaka ya hatia.
22Kisha kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kandoo dume mbele za Yahweh kutokana na dhambi aliyoitenda. Nayo dhambi iliyotendwa itasamehewa.
23Mtakapoingia katika nchi na kupanda aina zote za miti kwa chakula, kisha mtayahesabu matunda yatakayozaliwa kuwa yamekatazwa kuliwa. Tunda litakatazwa kwako kwa miaka mitatu. Halitaliwa.
24Lakini katika mwaka wa nne matunda yote yatakuwa matakatiifu, matoleo ya sifa kwa Yahweh.
25Katika mwaka wa tano unaweza kula tunda, ambalo umelisubiri ili kwamba mti uweze kuzaa zaidi. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
26Usile nyama yoyote amabayo damu ingalimo ndani yake. Usiulize kwa roho juu ya wakati ujao,
27Usitafute kuwadhibiti wengine kwa njia ya nguvu za kichawi. Msifuate tabia za kipagani kama vile kunyoa denge au kunyoa pembe za ndevu zeu.
28Usiukate mwili wako kwa ajili ya wafu au kuchanja chale juu ya mwili wako. Mimi ndimi Yahweh.
29Usimwaibishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo taifa litaangukia kwenye ukahaba na nchi itajawa na uovu.
30Utazitunza Sabato zangu na kupaheshimu mahali patakatifu pa hema langu la kukutania. Mimi ndimi Yahweh.
31Msiwageukie wale wanaoongea na wafu au roho wachafu. msiwatafute, la sivyo watawanajisi ninyi, Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
32Ni lazima usimame mbele za mtu mwenye mvi na uheshimu uwepo wa mzee. Yakupasa umwegope Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh.
33Mgeni anapoishi miongoni mwenu katika nchi yanu, usimtendee lolote lililobaya.
34Mgeni anayeishi pamoja nanyi ni lazima awe kama mwenyeji Mwisraeli mzaliwa anayeishi kwenu, na sharti umpende kama unavyojipenda wewe mwenyewe, ni kwa sababu wewe ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.

Read Mambo ya Walawi 19Mambo ya Walawi 19
Compare Mambo ya Walawi 19:13-34Mambo ya Walawi 19:13-34