Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 4

Luka 4:22-41

Help us?
Click on verse(s) to share them!
22Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”
23Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: Mganga jiponye mwenyewe, na pia mtasema: Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako.”
24Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake.
25Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.
26Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni.
27Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria.”
28Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.
29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.
30Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.
31Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.
32Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.
33Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:
34“We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!”
35Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
36Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”
37Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule.
38Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.
39Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia.
40Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.
41Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe u Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo.

Read Luka 4Luka 4
Compare Luka 4:22-41Luka 4:22-41