Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 11

Luka 11:18-37

Help us?
Click on verse(s) to share them!
18Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli?
19Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu ninyi.
20Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.
21“Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama.
22Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara.
23Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
24“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu fulani, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzikia. Asipopata, hujisemea: Nitarudi kwenye makao yangu nilikotoka.
25Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa.
26Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba waovu zaidi kuliko yeye; wote huenda na kumwingia mtu yule. Hivyo, basi hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko pale mwanzo.”
27Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri tumbo lililokuzaa, na maziwa yaliyokunyonyesha!”
28Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”
29Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
30Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.
31Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atashuhudia kwamba kina hatia. Yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni; kumbe hapa pana mkuu zaidi kuliko Solomoni.
32Watu wa Ninewi watatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, na watashuhudia kwamba kizazi hiki kina hatia. Hao watu wa Ninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na hapa pana mkuu zaidi kuliko Yona!
33“Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa pishi, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga.
34Jicho lako ni kama taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza.
35Uwe mwangalifu basi mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.
36Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utang'aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.”
37Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula.

Read Luka 11Luka 11
Compare Luka 11:18-37Luka 11:18-37